Thursday, 10 December 2015

TIBA ASILI YA MAFUA

Njia Rahisi za Kiasili za Kutibu Mafua.

Mafua ni ugonjwa unaosumbua watu kila mwaka, hasa yanapoanza kutokea mabadiliko ya hali ya hewa, kutoka msimu wa joto kuingia baridi au kutoka msimu wa kiangazi kuingiza masika. Ili kujikinga na ugonjwa wa mafua, ni lazima mwili uwe na kinga ya kutosha.


Orodha ya vyakula vifuatavyo vimeelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa kuimarisha kinga ya mwili na kupambana na maambukizi mengine kwa kuwa na kiasi kikubwa cha protini na virutubisho vingine.


SUPU YA KUKU
Supu ya kuku wa kienyeji inaelezwa kuwa na virutubisho vinavyosaidia kupunguza utokaji wa makamasi. Utapata virutubisho vingi zaidi ukitengeneza supu ya kuku kwa kuchanganya na mboga za majani. Weka chumvi kiasi kidogo katika supu hiyo.


VITUNGUU SAUMU
Vitunguu saumu vina kirutubisho aina ya ‘allicin’ ambacho kina uwezo wa kutoa kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali ya kuambukiza. Kitunguu saumu kinatoa kinga halikadhalika kinapunguza muda wa mtu kuumwa na mafua. Tumia kitunguu hicho kwa kupika kwenye chakula au kwa kutafuna punje zake.


CHAI
Chai, hasa ya kijani, (green tea) ina virutubisho vya kuimarisha kinga ya mwili. Utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na jarida moja la masuala ya virutubisho nchini Marekani (Journal of the American College of Nutrition) umeonesha kuwa watu wanaotumia chai kwa mpangilio maalum hawasumbuliwi mara kwa mara na mafua pamoja na magonjwa mengine ya kuambukiza, huwa salama na mafua au siku za kuumwa mafua hupungua kwa asilimia 36 ukilinganisha na wale wasiokuwa na kinga imara.


Hata hivyo, tahadhari inatolewa kwa watoto wa shule kutokupewa kiasi kingi cha chai kwa siku. Unywaji wa kikombe kimoja kwa siku kwa mtoto wa shule siyo mbaya. Kwa mtu mzima, asizidishe vikombe vitatu kwa siku. Ikumbukwe kuwa chai inapotumika kwa wingi kupita kiasi, huweza kusababisha pia tatizo la kukosa choo kwa muda mrefu. Kunywa kiasi kwa afya yako.


MACHUNGWA, PILIPILI KALI
Utafiti unaonesha kwamba ulaji wa vyakula vyenye Vitamin C kwa wingi kila siku husaidia kuondoa au kuzuia ugonjwa wa mafua. Miongoni mwa vyakula vyenye kiwango kikubwa cha Vitamin C ni pamoja na machungwa, mboga za majani aina ya Brokoli na pilipili kali.
Ili kupata kiasi kingi cha Vitamin C, inashauriwa machungwa yaliwe pamoja na nyama zake za ndani au kunywa juisi yake.


ASALI
Kama inavyojulikana, asali ni tiba ya matatizo mengi ya kiafya, miongoni mwa hayo ni pamoja na mafua. Asali inasaida kuondoa kikohozi na muwasho kwenye koo. Halikadhalika, asali inaweza kutumiwa na watoto wadogo kama dawa.


Watoto wanaoruhusiwa kutumia asali kama tiba ni wa umri kati ya miaka 2 hadi 5. Hawa dozi yao ni nusu kijiko kidogo cha asali, wenye umri wa miaka 6-11 wapewe kijiko kimoja kidogo na wenye umri kuanzia miaka 12 hadi 18, wapewe vijiko vidogo viwili vya asali wakati wa kulala.

MTINDI
Kutokana na kiwango kikubwa cha protini ilichonacho, Mtindi ni chakula kingine kinachofaa kuliwa na mtu mwenye mafua ili kupunduza siku za kusumbuliwa na ugonjwa kukohoa.

CHOKOLETI NYEUSI
Wataalamu wanakubaliana kuwa ulaji wa ‘chocolate’ nyeusi (dark chocolate) huimarisha kinga ya mwili, hivyo inapoliwa na mgonjwa wa mafua huweza kumpa ahueni mgonjwa kwa namna moja ama nyingine. Halikadhalika huwa kinga kwa maambukizi mengine.

PWEZA
Samaki aina ya pweza wana virutubisho vingi vya kuongeza kinga ya mwili yenye uwezo wa kupambana na bakteria pamoja na virusi vya mafua. Kiasi kidogo cha pweza, awe wa kukaangwa au kuchemshwa kama supu, anafaa kuliwa mara kwa mara kuimarisha kinga ya mwili.


VIAZI VITAMU
Kirutubisho aina ya ‘Beta-carotene’ huimarisha kinga ya mwili. Kirutubisho hicho huwa ni muhimu kwa ustawi na uimarishaji wa kinga mwilini na kinapatikana kwa wingi kwenye viazi vitamu na vyakula vingine kama vile karoti, maboga na mayai, (kiini).


Kwa ujumla, suala la kuimarisha kinga ya mwili ni muhimu kwa afya zetu. Ulaji wa vyakula vilivyotajwa hapo juu na vingine, unatakiwa kuwa ni wa mara kwa mara kama siyo wa kudumu, kwa sababu mwili unapokosa kinga imara, ni rahisi kushambuliwa na maradhi ya kuambukiza.

Kila dawa na Ugonjwa wake..
posted from Bloggeroid

CHAKULA NA UNENE - 4



SEHEMU YA 4:

MAMBO KUMI YA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUANZA SAFARI YA KUPUNGUZA UZITO

Nimekuwa nikitamka sentensi hii mara kwa mara kuhusu kupunguza uzito na laiti ungekuwa unaijua maana yake usingekuwa unasumbuka tena na uzito mkubwa kiasi hicho!
Napenda kurudia tena, Je upo tayari kuifuata? Najua kwa jinsi gani umekuwa ukijaribu kujinasua itakuwa na mara yako ya kwanza kuitilia maanani sentensi hii,
“Njia pekee yakupunguza uzito ni kuwa mwenye afya” Maana yake kama mwili wako unashambuliwa na changamoto mbalimbali hasa zinazoharibu shughuli za mwili na hatimaye mwili kushindwa kuendesha shughuli zake ipasavyo. Inapofikia hapo mwili wako hauwezi kupunguza uzito haijalishi unatumia nguvu kiasi gani.

Na njia pekee ili uweze kuwa mwenye afya na kuufanya mwili wako ufanye kazi katika misingi yake bila kuchanganyikiwa kiutendaji basi unatakiwa kuanzia leo ubadili chakula kinachoingia kinywani mwako na sio kupunguza kiasi cha chakula ambacho umekuwa ukiweka kinywani mwako. Kitendo cha kujinyima kula kunasababisha homoni kama adrenaline na noradrenalines (stress hormones) kutolewa kwa wingi na zinauwezo mkubwa wa kukusababishia hamu Zaidi ya chakula na uzito kuongezeka.

Hivyo kujinyima bila chakula kumeonyesha kunaongeza uzito kwa hali kubwa sana kulingana na tafiti zilizofanyika. Siri kubwa sio KUJINYIMA CHAKULA bali ni KUJITAHADHALI CHAKULA KINACHOINGIA KINYWANI MWAKO NI CHA AINA GANI NA KINA UBORA GANI KULINGANA NA TATIZO LAKO?
Unatakiwa kujua kuwa LISHE YA MTU ambaye hana uzito mkubwa au kitambi ni tofauti kabisa na yule mwenye uzito mkubwa na kitambi. Ndio maana basi inashangaza unapokuwa una ndoto ya kupunguza uzito lakini mlo wako unafanana na mlo wa watu wengine ambao hawana ndoto kama yako kiafya.

Basi leo nataka nizungumzie mambo kumi ambayo lazima uyafuate unapotaka kupunguza uzito wako. Na kama umekuwa ukitaka kupunguza uzito kilo kumi ndani ya siku 7 basi hizi Makala hazita kufaa kwani bado una fikra potofu ya kupunguza uzito bila kujali afya yako na ni bora kutoendelea kupoteza muda kusoma haya! Kama HUNA HARAKA! Basi endelea rafiki! Kama unapenda na unaamini kitendo cha kupunguza uzito ni safari ya polepole na hasa Zaidi unapotaka kupunguza uzito kiafya basi zingatia ushauri huu ambao nimekuwa nikikupatia.

1. USIHIFADHI CHAKULA NDANI MWAKO KILE AMBACHO UNAKIEPUKA
Moja ya kitu cha pekee ambacho utatakiwa ukizingatie ni kutokuwa na chakula chochote ambacho ni hatari kwa afya yako. Hata familia yako ijengee mazingira ya kuepuka tatizo maana siku akipata tatizo kama lako ni kazi sana kuliondoa kama unavyofikiria.
Napenda nikupe siri moja tu kwamba, endapo ukiweka mbali vyakula na vinywaji hatari kwa afya yako, unakuwa unajisikia uvivu kwenda na kuvifuatilia na hivyo hutaweza kuvitumia. Pia unaweza ukawa unauhitaji nacho lakini huna pesa uta ahirisha! Lakini endapo vyakula hivyo vimo ndani ni virahisi kutojizuia kuvitumia.
Hii hatua ni ngumu sana kwani nimekuwa nikiongea na watu wengi na wengi wao mtihani huu umewashinda kabisa. Hivyo endapo unauchukia uzito naomba unipe ahadi rafiki yangu kuanzia leo utakaa mbali na vyakula ambavyo ni hatari kwa afya yako

2. KULA CHAKULA BORA KABLA HUJALA CHAKULA AMBACHO UNAJUA SIO BORA KWA AFYA YAKO
Watu wengi sana hupenda kutumia vyakula ambavyo ni hatari kwa afya zao na hivyo wanapokutana na chakula bora hushindwa kabisa kumudu kula chakula hicho na hatimaye afya hudhoofika. Nataka nikwambie kuwa tafiti zinaonesha kuwa watu wengi wenye uzito uliokithiri wana kabiliwa pia na upungufu wa madini na vitamin muhimu mwilini maana hivyo ndivyo vinavyohakikisha shughuli zote za mwili zinatembea katika mwendo sahihi na wenye kukufanya mwenye afya daima. Hivyo basi kukosa baadhi ya lishe kunasababishwa na kutoa kipaumbele kwa vyakula ambavyo sio bora kwa afya yako. Hivyo hakikisha umekula matunda kwanza kama unataka kunywa soda yako kwa wale ambao huwezi kabisa kujizuia kutumia vyakula vyenye sukari nyingi ( Sugary drinks). Hapa naaamanisha hakikisha unatoa kipaumbele kwa chakula sahihi ndipo utumie chakula ambacho hata nafsi yako inajua sio salama kwa afya yako.

3. KULA CHAKULA BORA KWA AFYA YAKO PALE UNAPOKUWA UNA NJAA
Nimekuwa nikijiuliza sana watu wanao fanya kazi katika maofisi makubwa ya serikali kwa nini unene na uzito mkubwa umekithiri? Nimejitahidi kufanya tafiti hii na swala dogo sana nimekuja kuligundua ni kwamba hawana mazoezi muda mwingi wako na kazi na kibaya Zaidi wanakula vyakula ambavyo ni hatari kwa afya zao kwani hawana jinsi kwa sababu yumo ofsini.
Nimekuwa nikiona ofsi nyingi sana zinatumia vyakula hatari kwa afya yako, kama mikate na mchana unakula viazi vilivyo okwa na nyama ya kuku pembeni. Hii ni ishara kuwa unakula chakula ambacho sio bora wakati una njaa. Na pia niekuwa nikiona watu wengi sana wanapokuwa wananjaa basi ananunua au anafungua soda yake apate sukari kwanza huku akiendelea na kazi. Na bado anahitaji kupungua uzito! Umeona jinsi gani unavyo enda kinyume na zoezi zima la kupungua uzito? Nimekuwa nikiambiwa na wazazi wangu usemi “Ukitaka kizuri lazima ulipe gharama” Maana yake ukitaka kupungua uzito fuata mashart utafurahia kama wenzako wanaofuata mashariti ndio maana unatamani kuwa kama wao.

Pia hakikisha unaandaa chakula na unakuwa na muda sahihi wa kupata chakula ili pindi tu unapopata njaa upate chakula ambacho ni bora kwa afya yako ili utimize malengo yako. Changamoto ipo pale unapokuwa una njaa na hauna chakula ambacho unatakiwa ulishe mwili wako na hatimaye unaishia kula vyakula ambavyo ni hatari kwa afya yako.

4. EPUKA VYAKULA VYOTE AMBAVYO UNAONA UNAWEZA KUVIEPUKA NA USIVIJALI
Hapa wengi hujitahidi kuepuka kwa maneno na baada tu ya kutoka nje na marafiki zao hujificha na kutumia kile kitu ambacho nafsi inashuhudia kuwa ulikiacha. Naomba unapo amua kuvunja agano ujue utakuja unalipa gharama yake ya kutofikia malengo yako unayo yataka

5. BADILI MLO WAKO NA MWENENDO WAKO POLE POLE
Watu wengi wanaohitaji kupunguza uzito au kitambi siku zote huwa wana haraka kwani wanasahau kitambi na uzito mkubwa alivipata kwa muda mrefu. Hivyo hakikisha kwamba unafuata mashariti haya kama unahitaji kupunguza uzito wako kiafya na salama kabisa.
Na hivyo unajua kwa nini umekuwa ukijitahidi kubadili tabia na ujaribu kupungua na umeshindwa? Jibu ni dogo tu najua utashangaa! Lakini hata usishangae kwa sababu ni haraka zako za kufikia malengo yasiyo ya kiafya yanakukosesha mafanikio ya kuishi bila kitambi, hebu sikiliza! Ukitaka kuacha vyakula fulani jitahidi kuacha kimoja kimoja, na pole pole kwani watu wengi wameonesha kushindwa kuacha kutumia kitu fulani na kuishi maisha ya mazoezi kwa kujaribu kuacha vitu vyote kwa wakati mmoja. Nakushauri kuwa kama unataka kupunguza uzito basi anza kuacha tabia au chakula ambacho unajua ni hatari pole pole lazima utafanikiwa.

6. USIJIPONGEZE KWA VYAKULA
Watu wengi tunapopata pesa baada ya mihangaiko ya utafutaji huwa tunajipongeza! Na wengi wetu hujipongeza kwa nguo,chakula na sherehe maalumu kwa ajili ya pongezi hio. Jiulize wewe huwa unajipongeza kwa namna gani upatapo pesa? Kwa kwenda kula viazi vilivyo kaangwa kwa mafuta, kuku na pombe? Nakuomba upunguze au kuacha kabisa kujipongeza kwa vyakula kwani vinakupotezea mpangilio wa milo yako na hatimaye kuchanganya ubongo ulivyozoea katika kufanyia kazi chakula unachoweka mwilini mwako. Ukiweza hili hutarudi nyuma daima katika zoezi la kufikia mafanikio ya kuishi bila kitambi.

7. KUWA NA DAFTARI LA LISHE
Hili sio daftari la kuhesabu kiwango cha sukari unachokula kwa siku wala kuhesabu vipande vya karoti ulivyokula kwa siku. Hiki kitabu kinatakiwa kitumike kuandika na kuanisha maamuzi yako unayoyafanya unapotaka kupiga hatua na kuepuka kitambi. Mfano umechukua maamuzi ya kuacha kunywa vinywaji vyenye kemikali ya vionjo, rangi, radha na sukari basi umeamua kuwa unatengeneza juisi ya matunda na mboga za kijani ambapo utakunywa juisi hiyo ndani ya dakika 15 baada ya kutengeneza. Huu ni mfano wa kuandika mikakati yako ili kwamba ukikiuka kitabu hiki cha kumbukumbu ya maamuzi kitakushtaki. Kama una nia ya dhati najua tutafika endelea kutambua kuwa wengi wao wameridhika na uzito mkubwa na kitambi kwa sababu wanashindwa kumudu hatua hizi kwa sababu vyakula vimeshawadhuru na hawana tena mamlaka juu ya miili yao katika maamuzi ya vyakula gani na vinywaji gani anatakiwa atumie.

Najua umedhamiria hakikisha sasa unajiwekea malengo yanayotimilika kama unachukia hali hio ya kitambi.

8. JICHUNGUZE UNAKULA CHAKULA KIASI GANI NA KWA MUDA GANI
Watu wengi hawajali kabisa zoezi zima la kula, hata anapokuwa amemaliza kula ukimuuliza ametumia dakika ngapi hajui na hakumbuki kabisa...
Hii ni kwa sababu watu wengi hufanya zoezi hili bila kujitambua kuwa wanakula ambapo ni hatari sana kwani huwezi kuchukua maamuzi ya kuamua kuongeza lishe fulani na upunguze kitu fulani katika mlo wako. Na kumbuka hata ule muda wa kutafuna chakula chako kinywani kinasaidia sana vimeng’enya chakula (enzymes) kufanya kazi katika kiwango stahiki. Hivyo kuanzia leo kuwa mwangalizi wa zoezi lako unapokuwa unakula utajikuta unapata mabadiliko hadi utashangaa unapokuwa unaelekea kuondoa kitambi na kupunguza uzito wako

9. Jitahidi kula vyakula vya mafuta mazuri kwa wingi na protini kwa wingi na punguza ulaji wa kiwango kikubwa cha wanga.

Tafiti zinaonyesha kwamba vyakula vya protini vina uwezo mkubwa wa kusisimua mwili wako kuchovya Vipunguza hamu ya chakula (appetite suppressants) ambavyo ni leptin na kufanya kazi yake ya kukufanya kutokuwa mtu wa kula hovyo bila kukata kiu ya njaa.
Chakula aina ya pili kinachofanya kazi kama protini ni vyakula vyenye mafuta mazuri. Na hivyo basi tafiti zinaonyesha kuwa vyakula vya wanga hupunguza na kusababisha kutofanya kazi yake ipasavyo endapo tu unapokuwa unakula wanga kwa kiwango kikubwa kupita kiasi.
Napenda kurudia na kusema kuwa kipimo cha wanga kwa mtu ambaye ana kisukari au uzito mkubwa na kitambi ni tofauti sana na mtu ambaye hana matatizo kama hayo. Ndio maana tunashauri kupunguza vyakula vya wanga unapokuwa unataka kufikia malengo yako.
Kuanzia kesho nitafundisha aina kuu ya vyakula na utajua wewe mwenyewe chakula gani upange na ufike unapotaka.

10. WEKA MALENGO
Hadi hapa ulipo fikia ni asilimia 80 ya kufanikiwa kuondoa kitambi na uzito mkubwa au kutofanikiwa. Maamuzi yote yako ndani ya uwezo wako kwani ndiye unayetakiwa kupanga mikakati ya kuyatimiza yote ambayo umeyasoma katika elimu yangu hii ya afya.

Nimeamua kuongea hizi hatua kumi kwanza kabla sijagusia maada halisi ili kujua kama kweli hutaweza kupuuzia hatua hata moja. Kuna mwingine ataruka kwa kujidanganya katika nafsi yake kuwa haina haja ya kuzingatia vipengele vyote tabia hio haitaweza kukutimizia malengo yako kamwe.

Napenda nihitimishe hapa kwa siku ya leo kesho kutakuwa na mada fupi na iliyo jaa elimu nzito kuhusu mwanzo wa mlo sahihi na makundi ya vyakula kwa ujumla. Watu wengi wamekuwa wakinitafuta kutaka kuwatajia ni vyakula gani watumie wapungue. Lakini mimi sitapenda kuwakaririsha bali nataka muwe waalimu wa vizazi vyenu wote maana hadi sasa matatizo ya uzito mkubwa, kitambi, shinkizo la damu, kisukari yameshamiri zaidi hata ya magonjwa hatari ya kuambukiza. Na bado dunia inayumba kutokana na jinsi gani viwanda vinavyoendelea kufurahi kukosa ufahamu kwa jamii yetu hasa katika vyakula tunavyoweka kinywani.

Naomba tena kukuomba na kukupongeza kwa ushirikiano wako wa kuendelea kuwakaribisha watu wengi kushiriki jukwaa hili kwa kunifuatilia facebook katika ukurasa wangu "Masha Nutrition Health Care"

Asanteni kwa kujumuika nami.


0784925000
0767925000
0622925000 whatsapp
posted from Bloggeroid