Add caption |
Kuanza kufanya kazi kwa Hospitali ya Wilaya ya Kishapu kumeelezwa kuwa ni msaada mkubwa kwa wadau wa huduma ya Afya hususani wagonjwa kutoka ndani ya Wilaya ya Kishapu
Hayo yamethibitishwa na baadhi ya wagonjwa wanaoenda kupata huduma katika Hospitali hiyo ambayo ipo jirani kabisa na eneo la Halmashauri ya Wilaya.
Hospitali hiyo ambayo ni ya Serikali imekuwa msaada mkubwa na wagonjwa wamekuwa wakimiminika kwa wingi kutokana na baadhi ya makundi ya wagonjwa kupatiwa huduma bila malipo kutokana na sera ya Serikali katika kutoa Huduma ya Afya. Makundi hayo ni pamoja na wazee kuanzia umri wa miaka 60, akinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Mmoja wa wagonjwa aliyehojiwa na mwandishi wa makala hii alidai yeye anatokea kijiji ya Mwakipoya alidai yeye amekuja Hospitalini hapo kwa kuwa amesikia habari kutoka kwa baadhi ya watu waliowahi kutibiwa hapo kuwa wagonjwa wamekuwa wakipata huduma zote hususani Vipimo na Madawa.
Wagonjwa kutoka vijiji vya Wilaya za jirani za Maswa na Meatu pia wamekuwa wakifika Hospitalini hapo kujipatia huduma.
Mbali na makundi hayo yanayopata huduma bila malipo lakini pia makundi mengine yamekuwa yakijipatia huduma kwa gharama za kawaida ikiwemo familia zinazochangia mchango wa Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii(CHF) pamoja na wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya(NHIF)
Wakielezea mapungufu wanayoyaona mara wanapoenda kutibiwa Hospitalini hapo, baadhi ya wagonjwa wamedai Hospitali bado inaonekana kuwa na Watumishi wachache kwani muda mwingine wamekuwa wakishuhudia Muuguzi mmoja au wawili wakilazimika kuhudumia Wodi zote za Wanaume, Wanawake, Wazazi na hata sehemu ya Huduma ya Wagonjwa wa nje(OPD). Hivyo wagonjwa wameomba jambo hilo lifanyiwe kazi na mamlaka husika kwani wao(wagonjwa) wamefurahi kufunguliwa kwa Hospitali hiyo maana imekuwa ni msaada kwao na imewaepusha gharama za usafiri kwa wakaazi waliokuwa wakienda kupata Huduma katika Kituo cha Afya Kishapu kilichokuwa kikitumika zamani kwa wakaazi wote. Kituo hicho cha Afya kilichokuwa kikitumika zamani kipo umbali wa zaidi ya Kilometa 8 kutoka mji wa Mhunze.
Hospitali ya Wilaya ya Kishapu ilianza kufanya kazi katikati ya mwezi Novemba 2015 na ina majengo na vifaa vyote vya Huduma ya Wagonjwa wa Nje(OPD), Huduma za kulaza Wagonjwa(IPD), Wodi ya Wazazi(Maternity Ward), Jengo la Upasuaji na Mochwari.
Jina linalotumika kwa Hospitali ni Dr. Jakaya Mrisho Kikwete District Hospital