Showing posts with label UNENE NA KITAMBI. Show all posts
Showing posts with label UNENE NA KITAMBI. Show all posts

Sunday, 10 July 2016

Njia sahihi ya kupunguza Kitambi na Unene



Mtindo wa maisha, vyakula na shughuli za kila siku za mwanadamu ni baadhi ya vitu vinavyosababisha idadi kubwa ya wake kwa waume kuwa na uzito au unene kupita kiasi na wakati mwingine kuwa na vitambi.
Matatizo haya yamekuwa yakiwapata watu wa jinsia zote na kuwanyima raha wanawake wengi, ambao hufikia hatua ya kutumia mikanda maalumu ya kufunga tumbo au kuhangaika kupitia njia mbalimbali ili kupunguza kadhia hiyo kwao.

Kutokana na kuongezeka kwa tatizo hilo, kumezuka dawa nyingi zinazodaiwa kuwa na uwezo wa kupunguza vitambi na uzito mkubwa, lakini wataalamu wa afya wanaonya kuwa ni sumu.

Tafiti nyingi za kisayansi zinaonesha kuwa dawa hizi kwa kiasi kikubwa zina kemikali kama vile phentermine, sibutramine, phenolphthalein, caffein, hydroxycitric acid (HCA) na senna ambazo zina madhara makubwa kwa afya ya mwanadamu.
Dk. Phil McGraw anasema baadhi ya dawa hizo huathiri sehemu ya ubongo inayohusika na hamu ya chakula.  "Hamu ya chakula ni muhimu kwa ajili ya ubora wa afya na maisha.  Dawa yoyote inayoharibu hamu ya chakula kwa kipindi kirefu, inaweza kusababisha madhara ya kiafya", anasema Dk. Phil.
Mama mwenye uzito wa kilo 108, Doreen Shayo anasema amewahi kujaribu dawa za kupunguza mwili, lakini akapatwa na homa kali iliyohatarisha maisha yake baada ya wiki moja, hivyo alishindwa kuendelea na dozi hiyo.

"Nilishawishiwa kununua dawa hiyo ya kupunguza uzito na nilishauriwa kula mbogamboga, matunda na maji kwa wingi wakati wa dozi, sikuwa nakula wanga wala chakula kamili.  Nilipata homa ya ghafla madaktari wakanishauri kwamba dawa zile hazikuwa nzuri kwangu hivyo niachane nazo, wakati huo nilikuwa na kilo 120 lakini nilipungua kutokana na maelekezo ya madaktari", anasema Doreen.
Baadhi ya madaktari bingwa wa afya ya binadamu wanasema msukumo wa dawa hizo unaowafanya wahusika kuharisha mafuta mengi kwa wakati mmoja, ni njia isiyo sahihi ambayo pia huathiri baadhi ya viungo ndani ya tumbo, huku madhara yake yakijitokeza miaka kadhaa mbeleni.

Tabibu mmoja wa tiba mbadala anasema asilimia kubwa ya dawa za kupunguza kitambi na mwili kwa uharaka ni sumu.
"Mtu anapewa dawa anaharisha sana, swali la kujiuliza nini dawa inafanya tumboni na kusababisha kupata choo laini au kuyeyusha mafuta kwa muda mfupi?  Lazima tujue kwamba zina madhara baada ya muda, wengi wanauziwa vitu vibaya na mbegu fulani ambazo ni sumu halafu mwili unabadilika anaharisha sana, anaambiwa dawa ndio inafanya kazi yanatoka mafuta mengi, si njia sahihi ya kupunguza uzito wa mwili au kitambi."

Dk. Samuel Shita kutoka Hospitali ya Mwananyamala anasema kwa kawaida kuharisha humfanya mtu kupunguza maji mengi na chumvichumvi mwilini na hivyo huathiri kazi ya seli na mfumo wa fahamu.

"Dawa hizo nyingi hazijaruhusiwa kutumika na Wizara ya Afya na wala hazijathibitika kwamba ni sahihi kwa matumizi ya binadamu, lakini wanazitumia na madhara yake yanaanza kujitokeza baada ya kutumia mtu anaharisha sana na yeye anadhani ana mafuta lakini ule ni uteute unaokaa tumboni unaosaidia tumbo kufanya kazi.

"Utafiti unaonesha kuwa watu wanaopendelea kula katika migahawa mikubwa ndio wanaoongoza kuwa na miili mikubwa, teknolojia zipo na dawa zitumikazo lazima ziwe zimefanyiwa utafiti kwa zaidi ya miaka 10.  Kuna madhara mengi yanayoweza kuwakuta watu ikiwamo ya figo, moyo, ini na mishipa ya damu."


Dk Shita anasema kuna njia sahihi za kupunguza tumbo ambazo pia ni salama.  "Mtu anatakiwa kufanya mazoezi mepesi na matumizi sahihi ya vyakula, tunatakiwa kupunguza vyakula vya wanga kupita kiasi, sukari na mafuta.
Anasema soda, pipi na chocolate ni vyakula ambavyo havitakiwi kutumika kupita kiasi.

Tabibu wa tiba mbadala anazitaja hatua sahihi za kupunguza kitambi na kuondoa sumu mwilini akisema: "Kutumia juisi za matango na nyanya kila siku kwa muda wa mwezi mmoja sumu zote zinaondoka."
Hata hivyo, Mwaka anasema mtu anapokula chakula ni lazima kiishe tumboni kabla ya kuingiza kingine, vinginevyo anakuwa ametunza sumu mwilini kutokana na kuwa na mabaki mengi ya chakula cha takriban hata mwaka mmoja.

"Mfuko wa chakula una uwezo wa kutunza chakula kwa muda mrefu, ndiyo maana binadamu hufa akikosa chakula kwa siku nyingi.  Miongoni mwa vitu vinavyofanya uondoe sumu mwilini ni kufuata sheria za ulaji na njia za asili za kuondoa sumu hiyo na si njia za haraka kwani zina madhara," alisema.
Wataalamu wa masuala ya dawa Deborah Mitchel na David Dadson, katika kitabu chao kilichochapishwa mwaka 2002 cha "The Diet Pill Guide: The Consumer's Book of Over-the-Counter and Prescription Weight -Loss Pills and Supplements," wanasema:

"Ingawa ushahidi wa dawa hizi unazidi kuongezeka, bado watu wengi wanaaminishwa kwa uongo kuwa zina manufaa.  Hata hivyo, pia watu wanaendelea kuamini kuwa dawa hizi zinazotokana na mimea na ni dawa salama za asili zinazofanyiwa utafiti wa kina na kuthibitishwa na mamlaka za udhibiti na usalama wa dawa kama nyingine za hospitalini."

Namna ya kupunguza kitambi


Maji ya moto yakitumiwa kwa umakini yana uwezo wa kupunguza kitambi, tumbo au uzito mkubwa wa mwili kwa asilimia 60.
"Maji ya moto yana uwezo wa kupunguza tumbo kwa zaidi ya asilimia 60, unachotakiwa kufanya ni kuyachemsha yawe ya vuguvugu kiasi kunywa kati ya glasi nne mpaka sita na iwe ni katikati ya mlo mpaka mlo ndiyo maana kuna watu wanashauri unywe asubuhi au iwe katikati ya mlo wa jana usiku na ule utakaokwenda kuula baadaye.

"Lakini pagumu zaidi ni pale ambako kabla hujakwenda kupiga mswaki ndiyo unatakiwa kuyanywa haya maji.  Tunapata vitamin B12 ambazo zinazalishwa mdomoni wakati binadamu akiwa amelala na mojawapo ya vitamin hiyo ni pamoja na kusaidia msagiko (mmeng'enyo) ule wa vyakula."

Tatizo la wengi kukaa na vyakula kwa muda mrefu tumboni ni moja ya sababu pia ya kuwa na tumbo kubwa yaani kuwa na mafuta ya ziada tumboni na wengine wanakuwa na vyakula vingi wanavyoingiza kuliko wanavyovitoa.



"Asubuhi kabla hujapiga mswaki ukaondoa zile vitamin mdomoni zinywe pamoja na maji, kunywa maji ya vuguvugu glasi nne mpaka sita kila siku unapoamka asubuhi mfululizo mpaka siku 21, baada ya muda fanya hivyo kwa wakati mwingine na wakati ukifanya hivyo pia epuka vile vitu vitakufanya uendelee kuwa na tumbo ili unachokifanya kiweze kuwa na majibu na si kuoga na kujipaka tope," anasema na kuongeza kuwa kupunguza vyakula vya wanga ni njia mojawapo itakayomfanya mhusika kupata majibu ya haraka

NJIA SALAMA ZA KUPUNGUZA UZITO


Ukizungumza na watu wengi wanene watakwambia wanataka kujua njia ya kupunguza mafuta tumboni. 
Njia rahisi na salama ya kupunguza mafuta katika tumbo au kitambi ni ile ya kupangilia chakula na kufanya mazoezi.

Kama unataka kupunguza tumbo kwa haraka basi punguza kula vyakula vyenye wanga na badala yake tumia mbogamboga na matunda kwa wingi.

Vyakula kama viazi mviringo, wali, mkate hukaa tumboni kwa zaidi ya siku tatu, pia unywaji wa vinwaji vitamu vyenyw sukari nyingi unasababisha kuongezeka uzito na pia huongeza ukubwa wa tumbo.

Vyakula hivyo vinatakiwa kutumiwa kwa kiasi kidogo sana. Kuna wakati tumbo linajitokeza na kuwa kubwa kuliko kawaida hali hiyo inasababishwa na kula vyakula vya wanga kwa wingi, kutokunywa maji ya kutosha na pia kula bila ya mpangilio maalum.

Vyakula vya wanga na mafuta hufanya mtu kunenepa, acha au kupunguza kula vyakula hivyo.
Tumbo kuwa kubwa ni dalili kuwa chakula unachokula hakifanyi kazi inayotakiwa, kumekuwa na ziada mwilini na hii ziada inafanya mafuta ambayo hujiwekesha akiba katika maeneo mbalimbali ya mwili.
Kwa kuwa chakula hiki cha ziada huwa hakitakiwi, mwili hukibadilisha na kuweka akiba katika mfumo wa mafuta kitaalam kama glycogem.

Unaweza kukabiliana na kuzidi kwa protini zinazoyeyushwa na kuwekwa katika akiba kwa mfumo huo wa mafuta. Mtu mwenye tatizo hilo ni bora akapangilia mlo wake kwa siku kama ifuatavyo:
Asubuhi pata kifungua kinywa kilichokamilika, pata mlo wa mchana kama kawaida na usiku kula matunda tu kunaweza kufanya mwili wako uwe katika hali inayotakiwa.

Watu wengi wanatumia chakula cha wanga mwingi wakati wa usiku, muda ambao wanakwenda kulala na ziada ya chakula haifanyi kazi vizuri zaidi ya kujikusanya, kujibadilisha na kuhifadhiwa katika maeneo mbalimbali ya mwili hasa tumboni na kwenye makalio.

Mazoezi ya viungo husaidia kuchoma mafuta ya ziada katika mwili. Wanaume huwa na asilimia 8 hadi 20 ya mafuta katika mwili na wanawake ni asilimia 13 hadi 25.
Unapofanya mazoezi ya viungo unaongeza hewa ya oksijeni katika mapafu na wakati huohuo mwili nao unaunguza mafuta ili kutoa nguvu kwa mwili. 
Kwa ushauri zaidi wasiliana na daktari.